Galatians 3

Imani Au Kushika Sheria?

1 aNinyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa. 2 bNataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia? 3 cJe, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili? 4 dJe, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure! 5 eJe, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?

6 fKama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.” 7 gFahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Abrahamu. 8 hMaandiko yakitabiri kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, alitangulia kumtangazia Abrahamu Injili akisema kwamba, “Kwa kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.” 9 iKwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani.

Sheria Na Laana

10 jKwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.” 11 kBasi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.” 12 lLakini sheria haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” 13 mKristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.” 14 nAlitukomboa ili kwamba baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho.

Sheria Na Ahadi

15 oNdugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii. 16 pAhadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa wazao,” likimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako,” yaani mtu mmoja, ndiye Kristo. 17 qNinachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka 430 baadaye, haitangui Agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile. 18 rKwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kwa njia ya ahadi.

Kusudi La Sheria

19 sKwa nini basi iwepo sheria? Sheria iliwekwa kwa sababu ya makosa mpaka atakapokuja yule Mzao wa Abrahamu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Sheria iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. 20 tBasi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja.

21 uJe basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kwa njia ya sheria. 22 vLakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini.

23 wKabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe. 24 xHivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. 25 yLakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria.

Watoto Wa Mungu

26 zKwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27 aaKwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. 28 abWala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. 29 acNanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.

Copyright information for SwhNEN